Kuna
wanaume ambao kwa kutokujua wanadhani mwanamke anachohitaji ni ‘fidia’ baada ya
kuvunjiwa heshima, hivyo huwa wanawavunjia heshima wake zao na baadae kujitoza
‘fidia’ kwa kuwanunulia zawadi kubwakubwa wanawake hao.
Wanawake huwa wanapokea zawadi hizi,
lakini hii haina maana kwamba ndoa itaendelea kuwa ya amani na upendo. Mwanamke
hata kama atapewa dhahabu yote duniani, kama atajua kwamba mumewe hamheshimu,
ni wazi kwamba hatakuwa na furaha ya ndoa. Miongoni mwa mambo sita ambayo
mwanamke akiyakosa huhisi kutindikiwa na kukosa furaha ya uhusiano ni heshima.
Kama haki ya mwanamke hailindwi na
mwanaume, hata kama kuna kitu gani, ndoa ni lazima itakuwa ni ya kubahatisha.
Mwanume anapokuwa na uhusiano wa kipapenzi nje ya ndoa yake, mwanaume
anapomzuia mkewe kuamua masuala yake mwenyewe ambayo ni haki yake, kamwe
mwanamke hawezi kuridhishwa na hayo na hata kama ndoa imejaa watoto wazuri
wenye afya na akili na fedha nyingi zimeipamba nyumba yake.
Kama mwanaume ataonyesha kutojali
kuhusu matamanio au ndoto za mkewe kamwe mwanaume huyo asitarajie kuwa mkewe
atakuwa na upendo naye. Mwanamke huwa anatamani sana kuona mumewe anajali na
kuyapa uzito matamanio au ndoto za mkewe. Kwa mfano mwanamke anapoonyesha kwamba,
angependa kuanzisha shughuli labda ya biashara au wangependa wapate mtoto na
mwanaume akaonyesha kutojali kuhusu matamanio hayo, kamwe mwanamke hawezi
kutulia na kuwa na amani.
Kuna vitu au mambo ambayo mwanmke
anayahitaji maishani, mahitaji hayo ni mengi yakiwemo yale ya msingi katika
maisha na yale ya kawaida. Inatosha kusema kwamba, mwanamke anapogundua kwamba
mumewe hajali juu ya mahitaji yake huwa hajisikii vizuri.

Hapo ndipo tatizo ambalo ni la
upande wa pili huanza. Kwa maumbile mwanaume huwa anataka sana mkewe
akimuonyesha kwamba anamthamini na kumtambua. Labda hii inatokana na ubabe wa
asili wa wanaume ambapo kila wakati angependa kuona mwanamke akimgwaya na
kuonyesha kwamba anamtambua kama ‘mwokozi’ wa aina fulani.
Kama mwanamke anataka kumfanya
mumewe amsikilize na kujali matamanio na ndoto zake anachotakiwa kufanya ni
kumuonyesha mumewe kwamba anamthamini na kumtambua. Kwa mfano mwanaume
anapofanya jambo ambalo hata kama halina faida, lakini halina madhara, inabidi
mkewe aonyeshe kuzitambua juhudi hizo na kuonyesha kwamba, mume huyo
anajitahidi sana katika kufanya mambo yake.
Mwanaume anahitaji sana kuona
mwanamke akimsifu kwa juhudi anazofanya, iwe ni za kitabia au za shughuli.
Mwanaume anapokuwa na tabia nzuri, ni lazima mwanamke atafute kila njia ya
kumuonyesha kwamba ameitambua tabia yake hiyo, kamwe asimuonyeshe kwamba juhudi
anazofanya ni kupoteza muda. Pale ambapo mwanaume huonyesha heshima kwa mkewe
kwa kuzijali ndoto na matamanio yake ya kimaisha, huhitaji sana kuonyeshwa
kwamba heshima yake hiyo imepokelewa. Kwa kawaida mume anapotimiza wajibu wake
lazima mke naye atimize wajibu wake.
Kuna wakati na karibu mara zote,
mwanamke huwa anamlaumu mwanaume na mwanaume kumlaumu mwanamke kwa kila mmoja
kudhani kwamba mwenzake ndio chanzo cha matatizo. Hii ni kwa sababu wote wawili
hawajui namna nadharia hii inavyofanya kazi. Huyu anataka kuthaminiwa wakati
hampi mwenzake heshima na huyu anataka kupewa heshima wakati hamthamini
mwenzake.
Ili kuondoa kulaumiana huko inabidi
kila mmoja ajue wajibu wake, kwani kama mmoja ataanza kumpa mwingine kile
anachohitaji ni wazi huyu mwingine atajibu kwa kumpa mwenzake kile
kinachomstahili mwenzake ambacho ni heshima.
MC.RAY
WHATSAPP 0659/375263 INSTAGRAM MC.RAYMONDMUSHI FACE BOOK Raymond Mushi PAGE Rayshughuli |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni