1. Mwanaume Kicheche:
Hakuna mwanamke anayependa kuchezewa na
wanaume, labda tu kama anafanya hivyo katika juhudi zake za kujikwamua
kiuchumi, lakini pale mwanamke anapokuwa katika harakati za kutafuta mwanaume
ambaye kama mambo yakiwa mazuri wafunge ndoa, ni vyema akajiepusha na wanaume
vicheche wanaotongoza wanawake kwa lengo la kustarehe na kumaliza matamanio yao
ya ngono. wakati mwingine mwanaume mwenye tabia ya kuchezea wanawake anaweza
kumfuata mwanamke ambaye ametamani mwili wake na kujifanya eti amebadilika na
kuwa mtakatifu. Anaweza kujiweka katika mazingira yanayoonyesha kwamba
amebadilika ili kumvuta mwanamke. Shituka mwanamke, jasiri haachi asili
atakutumia kama condom na kisha kukutupilia mbali. Wanaume wenye tabia hizo ni vigumu
kubadilika. Inahitaji subira ya hali ya juu kujiridhisha kama kweli amebadilika
au anazuga ili apate anachokitaka
2. Mwanaume asiye na kazi
na asiyejishughulisha:
Mwaume asiye na kazi na asiyejishughulisha ni
mzigo usio na mwenyewe. Mwanaume asiyejishughulisha eti kwa sababu hajapata
kazi huyo hana malengo. Kukubali kuwa na uhusiano na mwnaaume wa aina hiyo ni
sawa na kuishi na mtu mfu anayetembea (dead alive), labda tu kama atakupa
sababu inayoingia akilini kuhusu kutokuwa kwake na kazi na kutojishughulisha
kwake. Kama atakuwa ni mtu wa kulalamika tu kwamba hakuna ajira na haonyeshi
dalili zozote za kuhangaika kutafuta hata vibarua ili kujikimu eti kwa sababu
ni msomi na badala yake anageuka kuwa ombaomba kwa ndugu zake na marafiki zake
Nawashauri wanawake muwaepuke wanaume wa aina hii kwani hawafai wanataka
kulelewa. Kama amekuona unafanya kazi au una vibishara vyako vinavyokuingizia
shilingi mbili tatu zinazokufanya uishi vizuri hapa mjini jua kwamba hicho
ndicho kilichomvuta kwako, ukikubali umekwisha maana atakukamua hadi tone la
mwisho kisha ahamie kwa mwingine, si kilichomleta kwako hakipo, sasa awe na
wewe kwa lipi....
3. Mwanaume asiyejiamini:
Kukubali kuwa na mahusiano na mwanaume
asiyejiamini ni sawa na kuishi na bomu ndani ya nyumba. Mwanaume asiyejihisi
kuwa yuko salama na mwenye mashaka muda mwingi kuhusu uhusiano wenu, hutawaliwa
na wivu wa ajabu ambao licha ya kukuletea fedheha kwa ndugu, jamaa na marafiki
zako, lakini pia anaweza kukudhuru au hata kukutoa roho siku moja. Wanaume
wasiojiamini mara nyingi ni watu wa kujitilia mashaka kuhusu hali zao za kipato
na uwezo wao katika tendo. Kuwa na mahusiano na mwanaume asiejiamini inabidi
uishi kwa akili na uchague maneno ya kuzungumza kila uwapo naye, kwani kila
neno utakalotamka litatafutiwa tafsiri na kitakachofuata ni tafrani, sasa tabu
yote ya nini..... Tupa kule hafai kwa mchuzi wala kwa kulumangia...
4.Mtoto wa mama:
Inawezekana mwanaume akalazimika kuishi
nyumbani kwao kwa muda baada ya kumaliza masomo au amepoteza ajira na akawa
bado hajapata ajira au hajapata shughuli ya maana itakayomwezesha kujitegemea,
hii inakubalika. Hata hivyo kama mwanamke anakutana na mwanaume ambaye anaishi
na wazazi wake na haonyeshi dalili za kutafuta kazi au shughuli yenye kipato
itakayomwezesha kuondoka hapo kwao na kujitegemea, usije ukajiingiza katika
uhusiano na mwanaume wa aina hiyo, itakula kwako, huyo ashakuwa kupe na
tegemezi, utakuwa ni mzigo wako na atakuganda kama luba na kupoteza bahati ya
kukutana na wanaume wenye mwelekeo wa maisha.
5. Mwanaume anayependa
kutukuzwa kama mfalme:
Unaweza kukutana na mwanaume aliyejipachika
kibandiko ufalme ambaye anapenda sana kuhudumiwa kama mfalme. Yaani anataka
afanyiwe kila kitu, na hajishughulishi kukusaidia kazi hata zile zinazotakiwa
zifanywe na mwanaume, yeye kazi yake ni kukaa sebuleni na kuangalia TV au
kusoma vitabu au magazeti huku akiagiza kila kitu asogezewe miguuni. Hawezi
hata kunyanyuka kufuata kitu anachotaka na badala yake ni kuamrisha aletewe.
Mwanaume wa aina hii ni wa kuepukwa kwani mwanamke kukubali kuwa na uhusiano na
mwanaume mwenye tabia za kupenda kutukuzwa kama mfalme ni kutaka kuishi kwa
msongo wa mawazo na jakamoyo na hivyo kufupisha umri wako wa kuishi hapa
duniani. Kinga ni bora kuliko tiba, ukikutana na mwanaume wa aina hii chapa
lapa hakufai..
6. Mwanaume mwenye
utititri wa watoto kila kona:
Mwanaume kuwa na watoto nje ya ndoa si jambo la
kushangaza siku hizi, lakini pale unapokutana na mvulana mwenye umri wa miaka
25 lakini ana watoto watatu kwa mama tofauti, mh! hapo sikushauri ujiingize
kwenye uhusiano na mwanaume huyo. Hata hivyo si lazima awe na miaka 25 tu hata
mwanaume mwenye umri mkubwa zaidi ya huo halafu ana watoto watatu au hata wanne
au zaidi kutoka kwa mama tofauti ni wa kuepuka. Hivi atakupa sababu gani
zilizomfanya akawa na watoto kwa mama tofauti kila kona ya mtaa mpaka umuelewe!
Kuwa na mahusiano na mwanaume aina hiyo ni kukaribisha shari nyumbani kwako
maana kila siku utapata wageni wanaokuja kudai hela za matumizi kutoka kwa
mumeo tena wengine watakuja kishari hasa na kukuharibia siku. Mh mh! sikushauri
mwanamke, sepa zako, bado nafasi unayo ya kumpata mwanaume mwingine mwadilifu.
Mwanaume anayejipenda mwenyewe ni kizungumkuti
kingine ambacho wanawake wanapaswa kujiepusha nacho. Utakuta mwanaume
anajipenda mwenyewe hakuna anachojali kuhusu mwenzi wake zaidi ya kujijali yeye
mwenyewe. Wanaume wenye tabia hii ya kujipenda wenyewe, huwa wana kawaida ya
kujijali wao wenyewe. Wanataka wavae nguo nzuri za thamani ili wao wapendeze na
si wenzi wao. Swala la kumjali mwenzi wake halipo katika vichwa vya wanaume wa
aina hii kabisa. Mwanamke sikushauri uingie katika moto huu.
8.Mwanaume bahili:
Unakutana na mwanaume mtoko wa kwanza tu
anakuchagulia aina ya chakula au kinywaji kwa kuangalia bei rahisi na wakati wa
kulipa anahesabia hela yake mfukoni, huyo ni janga. Utakapoingia katika
uhusiano na mwanaume wa aina hii atakusumbua sana na pia katika kupanga bajeti
nyumbani usishangae akihesabu finyango za nyama au vipande vya samaki jikoni.
Sikushauri mwanamke, we ingia mitini hakufai huyo........
9.Mwanaume chapombe mlevi
kupindukia:
Hakuna ubaya mtu kunywa pombe, hasa kama unajua
kiwango chako cha unywaji, lakini kuwa na uhusiano na mwanaume mlevi
anayekunywa pombe kupindukia kila siku non
stop 24/7 huyo hafai. Mwanaume wa aina hii ndio wale
wanaosema kunywa pombe watoto wakitembea uchi atajua mama yao. Hata siku moja
hawezi kuzungumzia maendeleo kwa ustawi wa familia, kwake utakuwa ni msamiati
mgumu.
10. Mwanaume mwenye
kisirani na asiyeweza kumuuwa nyoka akafa :
Mwanaume mwenye kisirani ni ngumu sana kuishi
naye. Mwanaume mwenye kisirani na anayependa kuweka vitu rohoni na asiyeweza
kusamehe ni janga. kuishi na mwanaume wa aina hii ni sawa na kuishi na explosive material ambayo
yakipata joto tu hulipuka. Mwanaume umetoka naye mtoko wa kwanza na kwa bahati
mbaya mhudumu wa mghahawa akasau kitu katika vitu mlivyoagiza akagomba kupita
kiasi na kuwakusanya mameneja wote wa mghahawa akiwemo mpishi mkuu akilalamika.
Na kama hiyo haitoshi mtaondoka hapo mghahawani njia nzima kambeba kichwani
mhudumu yule masikini aliyeghafilika mpaka mwisho wa safari yenu na huenda
akalala naye kichwani. Mwanaume huyo hafai kama gome la mgomba lisilofaa kwa
dawa ya miti shamba wala kuni, labda kwa kufungia ugoro. Huyo mpishe ajiendee
zake hakufai......
MC.RAY
WHATSAPP 0659/375263 INSTAGRAM MC.RAYMONDMUSHI FACE BOOK Raymond Mushi PAGE Rayshughuli |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni