![](https://lh3.googleusercontent.com/blogger_img_proxy/AEn0k_tv-qPid3fO4mPFp1rbdLm3EOgRIVbylnZTBpeIDaGUzPPYktnWyTcPkwCTrzwAEMlfZklUei2VlWXq3e4ddUBuKDfZ-iP0eb1-ojIGF8eUVQ9belLIa3CMoW3rgW88nq4t_pjtGrgzn4Mr8Yn-tjQ8SRxyovHqY9XQ5w9JiiJ-ci8_YRiozkmcgeYsnLXqZ68Tk9qKX2vwaLw9fOdGArCvROo7sSI89kDUExMrjtdi1WwbTM_8=s0-d)
Profesa Ibrahim Lipumba, kiongozi wa chama cha CUF nchini Tanzania akikabiliwa na mashitaka ya kuandamana bila kibali.
Kikao cha Bunge la Tanzania leo
kimevurugika kutokana na vurugu za baadhi ya wabunge waliokuwa
wakibishana kuhusu suala la kiongozi wa chama cha upinzani cha CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba kushambuliwa na polisi Jumanne kwa madai kuwa
alihusika katika maandamano kinyume cha sheria.
Hoja iliamshwa na
mbunge ambaye pia ni kiongozi wa upinzani aliyetaka suala hilo
lijadiliwe kwa dharura. Hayo yametokea huku Profesa Lipumba akifikishwa
mahakamani kusomewa mashtaka ya jinai.
Chanzo ni pale aliposimama
James Mbatia mbunge wa kuteuliwa kutaka suala la polisi kumshambulia na
kumdhalilisha Profesa Ibrahim Lipumba, kiongozi wa chama cha CUF
lijadiliwe kwa dharura bungeni humo.
Licha ya jitahada za Spika
Makinda kueleza kuwa suala hilo litajadiliwa kesho, kwa kuwa serikali
inahitaji muda wa kuwasilisha majibu, mambo yakavurugika.
Huku
wabunge wakiwa wamesimama wima wakishinikiza hoja hiyo ijadiliwe, Spika
Makinda aliendelea na msimamo wake wa kutaka hoja ijadiliwe Alhamisi
baada ya serikali kuwasilisha majibu, hapo ndipo mkorogano ulipozidi na
kuleta kutoelewana kati ya wabunge wa upinzani na Spika.
Spika
Makinda alilazimika kuahirisha kikao hicho mpaka jioni baada ya hali
kuwa ngumu, na hata jioni likaahirishwa tena mpaka kesho, Alhamisi.
Kiongozi
huyo wa upinzani inadaiwa alifika eneo ambako maandamano yaliyopangwa
kufanyika Jumanne yalikuwa yamepigwa marufuku, ingawa uongozi wa chama
cha CUF unadai Profesa Lipumba alikusudia kuwashawishi wafuasi wake
watawanyike kutii amri ya polisi ndipo akashambuliwa.
Wakati huo
huo Profesa Lipumba amefikishwa mahakamani mjini Dar Es Salaam ambako
amesomewa mashtaka ya kufanya maandamano bila kuwa na kibali.
Hata
hivyo kwa muda Profesa Lipumba alikimbizwa hospitalini baada ya afya
yake kudhoofika, ikidaiwa ni sababu ya kupigwa na polisi, madai ambayo
BBC haijaweza kuyathibitisha.
Hata hivyo alirejeshwa mahakamani
baada ya kupata nafuu, na kesi yake imeahirishwa na itatajwa tena
mahakamani tarehe 26 Februari 2015.
Ameachiwa kwa dhamana ya watu wawili kwa kiasi cha shilingi milioni mbili kila mmoja.