Kundi B katika michuano ya kombe la
mataifa ya Afrika lenye timu za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,
Tunisia na Cape Verde limeshindwa kuibua mbabe baada ya timu zote
kutoka sare ya kufungana bao 1-1.
Katika mchezo wa kwanza wa kundi
hilo Zambia iliumana na majirani zake Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo,
ambapo Zambia iliweza kujipatia bao la mapema ikiwa ni katika dakika ya
pili lililofungwa na Given Singuluma na kudumu hadi mapumziko. Hata
hivyo Yannick Bolasie aliweza kuisawazishia timu yake ya DR Congo katika
dakika ya 66. Hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa timu zote zilikuwa
zimeambulia goli moja na pointi moja.Timu ya Tunisia ilivaana na Cape Verde katika mchezo wa pili wa kundi B. Walikuwa ni Tunisia walioanza kujipatia bao katika dakika ya 70 likifungwa na Ali Moncer. Lakini dakika saba baadaye Cape Verde ilisawazisha kupitia mkwaju wa penalti uliofungwa na Almeida Ramos. Mchezo huu nao ulimalizika kwa sare ya 1-1, hivyo kutokuwepo mbabe wa kundi.
Leo ni mechi za kundi C ambapo Ghana itaonyeshana kazi na Senegal, zikifuatiwa na mchezo kati ya Algeria na Afrika Kusini.
Kundi A linaongozwa na timu ya Gabon ambayo iliirarua Burkina Faso 2-0 katika mchezo wa Jumamosi, huku wenyeji Equatorial Guinea wakitoka sare ya 1-1 na Congo.
CHANZO BBC
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni